Mwongozo Kuhusu Kujumuika kwa Njia Salama wakati huu ambapo kuna COVID-19

Multilingual Resources

Image

Iwe umepokea chanjo au hujapokea, ikiwa unapanga kuwaleta pamoja familia na marafiki msimu huu wa baridi, fikiria kuhusu unachoweza kufanya ili kujilinda na kuwalinda uwapendao dhidi ya COVID-19.

Kupewa chanjo ndiyo njia salama zaidi ya kujilinda na kuwalinda walio karibu nawe, hasa wale ambao bado hawastahiki kupokea chanjo. Chanjo ni madhubuti mno katika kukulinda usiugue vikali na kuzuia kifo. Hata hivyo, kuna hatari ya kuenea kwa maambukizi ya COVID-19 watu wanapokusanyika pamoja, iwe wamepokea chanjo au huwajapokea. Kupokea chanjo, kuvalia barakoa, kunawa mikono, na kukaa nyumbani ikiwa wewe ni mgonjwa ni hatua unazoweza kuchukua ili kusaidia kuwalinda wengine.

Mikusanyiko ya Hadhara

Kwa ujumla, unapokwenda kwa mikutano ya hadhara wakati huu:

 • Kupata chanjo ndiyo njia bora zaidi ya kujilinda dhidi ya kuugua vikali, kulazwa hospitalini au kufariki kutokana na COVID-19.
 • Valia barakoa. Iwe umepokea chanjo au hujapokea, waliofikisha umri wa miaka mitano na kuendelea, wanahitajika kuvalia vifunika-uso katika maeneo yote ya ndani ya umma, na katika shughuli za nje ambapo kuna watu 500 au zaidi, kama vile kwenye tamasha au michezo. Tunapendekeza sana kwamba watoto walio kati ya miaka 2 na 4 pia wavalie barakoa.
 • Kaa nyumbani ikiwa wewe ni mgonjwa au una dalili zozote.
 • Panga mapema. Endesha gari mwenyewe au tafuta njia mbadala ya kufika nyumbani ukijipata mahali pabaya au pasipo salama, kama vile baa iliyojaa watu ambao hawajavalia barakoa.
 • Sakinisha WA Notify kwenye simu yako mahiri. Utaarifiwa ikiwa huenda umetangamana na mtu aliyeambukizwa COVID-19, na iwapo umeambukizwa itawajulisha wengine bila kukutambulisha. WA Notify ni ya faragha kabisa na haikutambui wala kufuatilia unakoenda.

Mikusanyiko ya Faragha

Kabla ya kuwaleta watu pamoja

 • Pitia orodha ya wageni. Waza kuhusu unaowaalika. Je, kuna watu ambao huenda wakawa katika hatari kubwa ya kuambukizwa COVID-19, wakiwemo watoto wachanga ambao bado hawastahiki kupata chanjo? Je, unajua ikiwa wageni wako wamepokea chanjo au hawajapokea? Ikiwa hujui, ni muhimu kuuliza ili upange inavyostahili.
 • Panga mapema. Ikiwa kuna familia ambapo wanafamilia kadhaa hawajapokea chanjo, au ipo familia iliyo na mtu ambaye hajapokea chanjo na yuko katika hatari kubwa ya kuugua vikali kutokana na COVID-19, chaguo salama zaidi ni kufanya mkutano mtandaoni. Mkiamua kukutana ana kwa ana, wajulishe wazi marafiki na familia kuhusu jinsi usalama utakavyokuwa kipaumbele mkiwa pamoja.
 • Safiri salama. Ikiwa unapanga kusafiri ili kujumuika na familia au marafiki, tafadhali zingatia mwongozo wa usafiri wa CDC. Tahadhari unapoelekea katika eneo ambako msambao wa COVID-19 uko juu, valia maski na udumishe umbali wa futi sita (mita 2) kati yako na wengine ukiwa katika maeneo ya umma.
 • Fanyia mkutano nje. Mikutano ya nje ni salama zaidi kuliko ya ndani. Ikiwa ni lazima mkutano ufanyiwe ndani, chagua eneo ambalo lina hewa ya kutosha, kama vile chumba kilicho na madirisha yaliyo wazi.
 • Punguza idadi ya wanaohudhuria. Inapendekezwa kuwa na idadi ndogo ya wageni wa nje.
 • Iwe fupi.  Mkutano ukiwa mfupi unapunguza uwezekano wa kuenea kwa COVID-19. Mkutano mfupi pia hurahisisha kudumisha usafi wa mikono na sehemu zinazotumika.
 • Zingatia maslahi ya watoto. Huenda watoto wasidumishe umbali wa futi sita kati ya mmoja na mwingine, kwa hivyo kuvaa barakoa na kunawa mikono ni muhimu. Kumbuka: watoto walio chini ya miaka 2 hawapaswi kamwe kuvalia barakoa! Ikiwa mwanafamilia ana umri wa chini ya miaka 2 au hawezi kuvalia barakoa, punguza idadi ya watu ambao hawajapokea chanjo au ambao hali yao ya chanjo haijulikani.
 • Tathmini hali ya afya. Uliza ikiwa kuna yeyote ambaye amepata dalili kama vile kukohoa, joto jingi au matatizo ya kupumua ndani ya wiki 2 zilizopita. Waeleze wageni wajipime joto kabla ya kuwasili. Mtu yeyote aliye na joto jingi—au ambaye ana dalili zingine au anajua kuwa ametangamana na mtu aliye na COVID-19 ndani ya wiki mbili zilizopita—anapaswa kukaa nyumbani.
 • Pimwa. Iwe umepokea chanjo au hujapokea, unaweza kupunguza hatari ya kuambukizwa kwa kupimwa saa 72 kabla ya kujumuika na wengine. Siku ya kukutana, unaweza kujipima nyumbani. Hata ikiwa hujaambukizwa, bado ni muhimu kuzingatia tahadhari zingine za usalama zilizoelezwa katika ukurasa huu.
 • Sakinisha WA Notify kwenye simu yako mahiri. Utaarifiwa ikiwa huenda umetangamana na mtu aliyeambukizwa COVID-19, na iwapo umeambukizwa itawajulisha wengine bila kukutambulisha. WA Notify ni ya faragha kabisa na haikutambui wala kufuatilia unakoenda.

Wakati wa mkutano wa faragha

 • Valia barakoa. Ikiwa unajumuika sehemu ya ndani na watu wasio wa familia yako, inapendekezwa kila mtu avalie vifunika-uso, isipokuwa iwe wahudhuriaji wengi wamepokea chanjo kikamilifu. Kuwa na barakoa za ziada kwa wale ambao huenda hawana.
 • Nawa mikono. Iwapo hakuna sinki ya maji, tumia sanitaiza ya mikono.
 • Zingatia nafasi kati ya mtu mmoja na mwingine na watu wasikaribiane. Ikiwezekana kaa umbali wa futi 6, haswa kati ya watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa COVID-19 au baina ya watu ambao bado hawajapokea chanjo kikamilifu.
 • Fungua madirisha. Hakikisha madirisha yako wazi katika vyumba ambako watu wamekusanyika ili pawe na hewa ya kutosha.
 • Safisha. Safisha sehemu zinazotumiwa mara kwa mara kabla, wakati wa, na baada ya mkutano.

Baada ya mkutano wa faragha

 • Nawa mikono (tena). Nawa kwa sekunde 20 ukitumia sabuni na maji.
 • Safisha. Tumia maji na sabuni kisha kiua-viini kusafisha sehemu zote ambazo huenda zimeguswa na wageni kama vile meza, kaunta, mikono ya milango na sehemu za choo zinazoguswaguswa.
 • Angalia dalili. Ikiwa una dalili zozote, nenda upimwe. Waarifu waliohudhuria ikiwa mmoja kati yao ameambukizwa. Pata maelezo zaidi kuhusu hatua unayopaswa kuchukua ikiwa umetangamana mtu aliyeambukizwa.